Chama cha Viziwi Tanzania CHAVITA kimeiomba Serikali kutekeleza kwa vitendo mikataba yote ya kimataifa iliyoiridhia na kuisaini ikiwemo inayohimiza kila raia kuwa na haki ya kupata habari.

Miswada mingi iliyopitishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kutungiwa Sheria bado haijaanza kutekelezwa hali inayowapa wakati mgumu Viziwi kupata habari.

Katika mafunzo ya lugha ya alama kwa matabibu, wauguzi na watoa huduma kwenye hospitali, zahanati na vituo vya afya jijini Mwanza, Afisa Jinsia wa Chama cha Viziwi Tanzania Lupi Maswanya anasema inashangaza kuona Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo viziwi hawana haki ya kupata habari kupitia Televisheni.
Amesema Viziwi wanalipa kodi kama raia wengine lakini suala la kupata habari kwao ni kitendawili.

Kuhusu suala la afya kwa Viziwi wanapokwenda Hospitali kupata huduma, Lupi amesema hiyo ni changamoto kubwa kwao.

Mkufunzi wa Lugha ya alama anayesimamia kitengo cha Lugha hiyo katika chuo kikuu cha Dar es Salaam Malise Swila amesema tangu Rais John Magufuli aingie madarakani mwaka mmoja uliopita, Viziwi hawaelewi anatoa maagizo gani anapolihutubia Taifa kwa kuwa hakuna mkalimani anayefikisha ujumbe kwao.

Baadhi ya matabibu, wauguzi na watoa huduma katika hospitali, zahanati na vituo vya Afya wanazungumzia umuhimu wa lugha ya alama kwa ajili ya mawasiliano na Viziwi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here