Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imekamata shehena ya Sukari na Mafuta yenye thamani zaidi ya shilingi milioni mia nne ambazo zinaingianchini kutoka mataifa ya India na Brazil bila kulipa ushuru.

Shehena hiyo imekamatwa mkoani Lindi katika wilaya ya Kilwa ikiwa katika stoo ambapo hubadilishwa na kuwekwa katika vifungashio vyenye nembo za makampuni ya hapa nchini na kupelekwa sokoni.

Shehena ya bidhaa ambazo huingia hapa nchini kwa kupitia bandari bubu kutoka katika mataifa mbalimbali yakiwemo India na Brazil, na kuhifadhiwa katika jengo ambapo hubadilishwa kutoka katika vifungashio halisi na kuwekwa katika vifungashio vya makampuni kama Kagera Sugar,Mtibwa Sugar, Ndoo za mafuta ya Koree na nyinginezo.

Jengo hilo ndilo limegeuka na kuwa kiwanda cha sukari zinazozalishwa hapa nchini likiwa na kila aina ya mfuko wa kampuni za Sukari na ndoo za mafuta ikiwaaminisha watu kuwa ni bidhaa kutoka katika viwanda hivyo.

Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi na mawasiliano kwa umma kutoka mamlaka ya mapato TRA Richard Kayombo amesema athari zitokanazo na wafanyabiashara wakwepa kodi ni kubwa kwakuwa inakwamisha maendeleo ya nchi.

 Kayombo ameelezea kuibuka kwa bandari bubu zaidi ya 11 katika mkoa wa Lindi ambazo zimekuwa zikiingiza bidhaa mbalimbali kutoka katika mataifa ya nje na kulisababishia Taifa hasara.

Mmiliki wa kiwanda hicho bubu, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humu huku mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wakiendelea kuwasaka wale wote wanaotumia bandari Bubu hapa nchini kuingiza Bidhaa kinyume cha sheria.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here